contact


I made this widget at MyFlashFetish.com.

Wednesday, September 21, 2011

UKWELI KUHUSU MIGOGORO YA CHUO CHA USTAWI WA JAMII

Kwa takribani miaka minne sasa, kumekuwepo na mvutano kati ya Taasisi ya ustawi wa jamii (ISW) na Baraza la taifa la Elimu ya juu na ufundi (NACTE), kuhusu masuala ya taaluma katika taasisi hiyo. Mvutano huo uliwasukuma baadhi ya wahadhiri katika taasisi hiyo kushinikiza menejimenti yao kutekeleza mapendekezo ya baraza hilo kuboresha taaluma, lakini kilichowakuta wahadhiri hao, licha ya juhudi zote zilizofanywa na vyombo mbalimbali kujaribu kurekebisha mambo katika taasisi hiyo, bodi ya chuo iliridhia kuwafukuza kazi wahadhiri 21 mnamo agosti 21 mwaka huu, ambao kosa lao pekee kubwa ni kutaka taaluma iboreshwe katika chuo hicho

Wahadhiri hao wamefukuzwa kwa madai kwamba waliendesha mgomo usio halali na kukaidi maagizo ya mamlaka za juu


Mambo bado si shwari katika taasisi hiyo, mpaka sasa hakuna maboresho yoyote ya maana ya kitaaluma yaliyofanyika,  bali kinachoendelea pale ni migogoro ambayo hatma yake ni kuzalisha wahitimu walio chini ya kiwango wasioweza kushindana vyema katika soko gumu la ajira nchini


Ukweli ni kwamba, kiini cha migogoro ni taasisi kuendelea kupuuza maagizo ya NACTE. kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kwamba barua za NACTE zenye kumbukumbu NACTE/ DA/ 31/655/Vol 1./92 ya june 19/ 19/ 2010; zinaonyesha taasisi ya ustawi wa jamii ilipewa maagizo ya kufanya maboresho ili kukidhi matakwa ya ithibati yanayokubalika NACTE

Kwa mshangao, menejimenti iliamua kukaidi maagizo hayo ya NACTE. Na hili ndilo pia lililosababisha wahadhiri watatu waandamizi wa chuo hicho -Dk Mihanja, Dk Matiku na Dk Kitojo kujiuzulu kazi mwaka 2007.


Ukaidi huo ulisababisha taasisi kuzuiliwa kujihusisha na udahili wa programu za ngazi ya cheti, stashahada na shahada (certificate, diploma, degree programs) ilipofika April 2011, kwa kuwa ilishindwa kukidhi matakwa ya ithibati ya kwanza iliyoidhinishwa na NACTE kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2006-2011


Kwa barua hizo taasisi ilipewa muda mpya wa kuandaa mitaala na kurekebisha mfumo wa utawala hadi ifikapo septemba 2011 ili warudishiwe haki ya kuendesha program hizo, mpaka wiki mbili zilizopita hilo lilikuwa halijatendeka

Kwa ufupi, si kweli kwamba tatizo la taasisi hiyo lilikua ni hao wadhahiri waliofukuzwa kazi kama inavyodaiwa, wao walikuwa wakipigania taasisi hiyo kutii maagizo yaliyotolewa na NACTE. Si kweli kwamba waliachishwa kazi kwa kufanya mgomo usio halali, na si kweli kwamba kwa kuwafukuza kazi, hali ya kitaaluma ya taasisi hiyo itaboresheka,  ni mpaka hapo hilo litakapozingatiwa, hali ya kitaaluma ya taasisi hiyo haiwezi kuwa shwari, kwa sababu wahitimu wa taasisi hiyo wataendelea kuwa chini ya viwango na ajira zitaendelea kuwakimbia


menejimenti ya taasisi hiyo imekiuka haki za msingi za wafanyakazi walioachishwa kazi bila kufuata kanuni za ajira za taasisi ya ustawi wa jamii (staff regulation) na sheria ya kazi Na.6 ya mwaka 2004, na kwa mujibu wa katiba ya nchi, pia imewadhalilisha wadhahiri hao walioachishwa kazi wakipigania maslahi ya taasisi, maslahi ya wanafunzi na maslahi ya umma mzima wa Tanzania

No comments:

Post a Comment